HomeResourcesSabbath School quarterly

Msukumo wa Roho Mtakatifu

01/06/2026

Alipofikiria kuhusu umbali uliokuwepo kati yake na mke wake, alijua kwamba alikuwa amekosea. Alikuwa amekosa huruma na mwenye ukali, na alisema mambo aliyoyajutia. Lakini wazo lake lililofuata lilikuwa, Je, hakustahili hilo hata kidogo?

Je mchakato huu wa mawazo si mgeni kwako? Ni rahisi kubadilika kutoka kwenye hisia za majuto hadi kuhalalisha mawazo na matendo yetu. Si rahisi kila wakati kusema, Samahani … tunapokosea, lakini hili ni jambo muhimu sana katika kujenga upya au kuimarisha uhusiano wowote.

Hali hiyo hiyo inatuhusu sisi na Mungu. Roho Mtakatifu mara nyingi hutusukuma kufikiria kuhusu dhambi tunazotenda. Mioyo yetu hubadilishwa kwa sababu ya misukumo hiyo, lakini ni rahisi kuikataa ile sauti tulivu na nyororo tunapojaribu kuhalalisha sababu ya kutenda kwetu. Mojawapo ya majukumu ya Roho Mtakatifu ni “atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi” (Yohana 16:8). Ni zawadi ya ajabu jinsi gani kutoka kwa Mungu (Luka 11:13), kwani tunahitaji usadikisho kama huo ili kurekebisha umbali unaoweza kujitokeza katika kutembea kwetu pamoja Naye!

Tafakari juu ya kazi ya Roho Mtakatifu katika mchakato wa kuturejesha tena kwenye Mzabibu (Yohana 15:4). Mara nyingi tunahuzunika kwa sababu matendo maovu huleta matokeo yasiyofurahisha kwetu; lakini hii si toba. Huzuni ya kweli kwa ajili ya dhambi ni matokeo ya kazi ya Roho Mtakatifu. Roho hufunua kutokushukuru kwa moyo ambao umempuuza na kumhuzunisha Mwokozi, na hutuleta katika toba msalabani. Kwa kila dhambi Yesu hujeruhiwa tena; . . . tunaomboleza kwa ajili ya dhambi ambazo zimemletea maumivu. Maombolezo namna hii yatasababisha kuachana na dhambi. —Ellen G. White, Tumaini la Vizazi Vyote, Sehemu ya Kwanza, uk. 279-280.

Ukweli ni kwamba hatuwezi kukua katika uhusiano wetu na Mungu wakati dhambi tulizozichagua na kuzithamini zinasimama kati yetu na Yeye. Sote tumepungukiwa na utukufu wa Mungu, lakini tunaweza—na tunapaswa—kutubu dhambi zetu wakati ambao Roho Mtakatifu anazileta akilini mwetu (Waefeso 4:30).