HomeResourcesSabbath School quarterly
Mungu Katika Uumbaji
08/04/2026
Pengine unajua kwa kukariri maneno ya kwanza katika Biblia: “Hapo mwanzo Mungu.” Katika Kiebrania, neno linalotumika hapa likimaanisha Mungu ni Elohim. Ingawa neno hili laweza kutumiwa kuzungumza juu ya “miungu” ya uongo, linaporejelea Mungu mmoja wa kweli, linafafanua Muumba mweza wa yote, mwenye uwezo wote kuhusiana na uumbaji wote; Mungu mkuu ambaye yuko nje ya ufahamu wetu lakini anatawala kila kitu. Yeye ni mwenye nguvu sana kiasi kwamba anapozungumza, kitu kinaundwa kutokana na sauti yake tu.
Lakini katika sura inayofuata, Mwanzo 2, kunatokea jina tofauti la Mungu: YAHWEH. Jina hili linaungana na Elohim (Yahweh Elohim), Mungu yule yule mweza wa yote, Mwenyezi; lakini jina Yehova ndilo jina binafsi mahsusi la Mungu pekee wa kweli, ambalo mara nyingi hutumika kukazia kwamba Mungu ndiye Mungu wa agano, katika uhusiano wa upendo na watu Wake aliowaumba.
Hapa, kwenye Mwanzo 2:7, tunaweza kumfikiria Mungu akipiga magoti ili kuumba mwanadamu wa kwanza kutoka ardhini kwa mikono Yake mwenyewe. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Huyu ni Mungu anayekuja karibu kabisa — karibu kiasi kwamba anapulizia puani kwa Adamu pumzi ya uhai. Jina hili, Yahweh, linawasilisha taswira ya karibu zaidi ya Mungu, lakini Musa anatumia majina yote mawili kwenye sura mbili za kwanza za Biblia katika kutuelezea tabia hizi mbili za Mungu.
Inashangaza kiasi gani! Hapa tunaona hali hii ya Mungu kupita uwezo wa kibinadamu akiwa kama Elohim, na hali Yake ya kuwepo ndani kabisa kati yetu pia kila mahali, ukaribu Wake nasi kama Yahweh. Ni jambo zuri kwetu kiasi gani kufikiria juu ya vipengele hivi vya tabia ya Mungu: udhibiti, utawala wake wa kila kitu na ukaribu wake kwetu. Kama Paulo alivyosema kwa Waathene katikati ya Areopago “ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.“ (Mdo. 17:27, 28).
Ni muhimu tuendelee kutafuta picha yenye ulinganifu, iliyo wazi, ya Mungu msingi ukiwa katika kile Biblia inachotuambia kuhusu tabia ya Mungu ili tupate kukua katika uhusiano na Yeye. Hii ndiyo sababu ni muhimu kusoma sehemu zote za Biblia badala ya kukaza macho kwenye sehemu moja tu. Kwa kweli, kadiri tunavyozidi kujifunza kuhusu tabia ya Mungu, ndivyo tutakavyozidi kujifunza kumpenda.