HomeResourcesSabbath School quarterly
Kemea, Tubu na Thawabu
30/03/2026
“Wote niwapendao, mimi nawakemea, na kuwarudi,” Yesu anatuambia kwenye Ufunuo 3:19. “ ‘Basi uwe na bidii, ukatubu.’ ”
Hakuna hata mmoja kati yetu, hata kwa sekunde moja, angeweza kusema kwa usahihi kwamba Bwana Yesu hatujali wala hajali mustakabali wetu. Ingekuwa rahisi zaidi kiasi gani kwa Yesu kuachilia ubinadamu na asiipitie njia ya maumivu aliyoichagua hapa duniani. Ni kwa usahihi kabisa kwamba anatupenda kwa upendo wenye kina sana kiasi cha kutukemea kutokana na hali yetu ya sasa. Yeye anataka kuwa na uhusiano imara zaidi, wenye kina zaidi na sisi. Yeye haridhishwi na mitazamo yetu inayoyumba, mitazamo yetu ya "Nitamjia Yeye pale nitakapomhitaji."
Badala yake, Yesu anatukemea kwa manufaa yetu. Yeye anatuambia tutubu. Lakini hatuwezi kutubu tusipotambua kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa. Licha ya hivyo, ametuambia kwa umahsusi kabisa kosa letu: tunadhani kuwa tu matajiri, lakini kwa kweli sisi ni yule aliye “ ‘mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi' " (Ufu. 3:17).
Hii ni lugha nzuri sana yenye kuweka taswira isiyo ya kawaida. Mungu wa ulimwengu anataka kuketi chakulani pamoja nawe, pamoja nami. Anatamani ushiriki wa pamoja na mazungumzo katika chakula kizuri, Haya ni maelezo ya uhusiano wa karibu, wa kudumu, na Bwana Yesu anatualika tuwe na uzoefu huu pamoja Naye.
Yesu anasimama kwa subira akingoja na kubisha hodi kwenye mlango wa moyo wako. Pengine umeona picha za mwonekano huu “katika vitabu vya watoto-Mwokozi mrefu, mwenye neema, akigonga kwa upole. Yeye hakuingilii na kukulazimisha kuzungumza Naye. Yeye hakuvamii katika wakati wako au maisha yako yenye shughuli nyingi. Muda ni mfupi, kwa hiyo, ukimsikia, fungua mlango. Atakuwepo ili kuingia maishani mwako.
Sitiari hii inaonesha namna ya uhusiano ambao Yesu anataka uwepo kati Yake na kila mmoja wetu. Lakini siku moja, utakapokutana na Yesu ana kwa ana, utakapoiweka chini taji yako miguuni pake ukimsujudia na kumsifu pamoja na maelfu kwa maelfu wengine katika ibada kwa Muumba (Ufu. 4:9-11; Ufu. 5:11-14), utakapojaribu kutupa mawazo yako nyuma kwenye majaribu ya kidunia na kuona kwamba yanapotea na kuonekana kuwa hafifu kiasi cha kukosa maana — unadhani wakati huo utajuta hata kidogo kwamba ulitumia muda uliokuwa nao na Yesu hapa duniani?