HomeResourcesSabbath School quarterly

Umeponywa

08/06/2026

Fikiria msongamano wa watu katika pwani ya Galilaya. Walikuwa wakimsubiri Yesu arudi tangu asubuhi na mapema, na anaposhuka kutoka kwenye mashua, wanamsogelea kwa karibu, wakimfuata hadi kijiji cha Kapernaumu. Ghafla, Yairo, mkuu wa sinagogi, anatokea na kumsihi Yesu aende kumponya binti yake.

Mmoja wa watu waliokuwa katika umati ni mwanamke aliyekuwa mgonjwa kwa miaka mingi. Alitumia fedha zake zote kwa madaktari, lakini “kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya” (Marko 5:26). Alikuwa amesikia habari za Mtu huyu mkuu kutoka Galilaya, na kwa tumaini moyoni mwake, anakusanya nguvu kidogo alizokuwa nazo kuondoka nyumbani kwake asubuhi hiyo ili kuungana na umati. Msongamano wa watu ulisonga kiasi cha kukosa hewa alipojikokota kumkaribia Yesu. Kisha, katikati ya kusukumana na Kusongamana, anamwona. Anajitia moyo: “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona” (Marko 5:28)

Tukio hili linaonesha kujali kwa Yesu na huruma kwa wagonjwa na waliotengwa, na wale ambao kwa kawaida wanaonekana kutozingatiwa. Wengi siku hiyo walikuwa wakimsogelea Yesu kwa karibu walipokuwa wakisukumana pamoja na umati, lakini ni mmoja tu aliyemfikia kwa makusudi ili apokee baraka aliyokuwa akihitaji kwa hamu. Hata hivyo, si mguso wake uliomponya; bali ni imani yake iliyomponya (Marko 5:34). “Mwokozi aliweza kutofautisha mguso wa imani na mguso wa kawaida wa msongamano wa watu. —Ellen G. White, The Desire of Ages, uk. 344. Vazi la Yesu halikuwa na nguvu maalum; bali ni imani ya mwanamke huyo na uamuzi wake wa kumsogelea na kumgusa ndiyo iliyomponya.

Mwanamke uyo dhaifu, katika mateso na dhiki yake, angeweza kubaki kitandani nyumbani asubuhi hiyo, lakini badala yake aliamua kwa makusudi kumtafuta Yesu kwa tumaini la kuponywa. Kumwona akiwa mbali hakukutosha; alimsogelea kwa karibu.

Yesu anatuita kufanya vivyo hivyo leo. Anasema, “ ‘Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, Nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu’ ” (Mathayo 11:28, 29).