HomeResourcesSabbath School quarterly

Ayubu

09/06/2026

Tunapofikiria kuhusu changamoto katika Biblia, Ayubu huenda ndiye mtu wa kwanza anayekuja akilini. Hakupoteza tu mali zake zote (Ayubu 1:14-17) bali pia alifiwa na watoto wake (Ayubu 1:18, 19) na kupoteza afya yake (Ayubu 2:7). Kisha mke wake alijaribu kumshawishi amkufuru Mungu na afe (Ayubu 2:9).

Baada ya muda, rafiki watatu walikuja kuketi na Ayubu. Walishtushwa sana na mwonekano wake kiasi kwamba walikaa naye pasipokuzungumza chochote kwa siku saba (Ayubu 2:13). Hatimaye walipoanza kuzungumza, walijaribu kutoa sababu za kibinadamu kuhusu sababu ya taabu hiyo kubwa kumkumba Ayubu, lakini kwa kufanya hivyo, waliongeza mateso yake bila kukusudia. Rafiki hao watatu walimlaumu, wakisema lazima kuna dhambi iliyofichika katika maisha yake anayopaswa kutubu (Ayubu 8, 11, 15), hata wakasema, “ ‘Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotevu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu’ ” (Ayubu 18:21).

Haidhuru matukio ya kusikitisha yaliyomzunguka na ukweli kwamba hakuyaelewa, Ayubu alibaki kuwa mwaminifu. Alishikilia imani yake. Hakumlaumu Mungu wala kumkufuru. Badala yake, alipojaribiwa kumlaumu Mungu, alitamka: “ “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe’” (Ayubu 1:21).

Sisi pia tunaishi katikati ya vita hii hii. Shetani hutuletea maumivu, mateso, kufiwa, na shida kama sehemu ya mpango wake wa kupotosha taswira yetu ya Mungu mwenye upendo. Katika nyakati kama hizo, tunaweza kuitikia kwa njia moja kati ya mbili: kumlaumu na kumkataa Mungu, au kushikamana naye kwa nguvu zetu zote. Ingawa vita ni kali, tunapaswa kukumbuka kwamba, kwa mtazamo wa milele, matatizo yetu ya muda ni majaribu ya muda tu (2 Wakorintho 4:16-18). Kuna mengi zaidi katika taswira kuliko tunavyoona hapa na sasa, na mojawapo ya changamoto kubwa kwa muumini ni kumtumaini Mungu hata katika nyakati za giza kabisa. Mungu ametufunulia kwa njia nyingi uhalisia wa upendo Wake. Tunapaswa kung’ang’ania ukweli huu muhimu—wa upendo wa Mungu—hata pale ambapo hatuuoni kwa wakati huo.