HomeResourcesSabbath School quarterly

Ni Kitamu Sana!

30/04/2026

Fikiri juu ya kitindamlo unachokipenda zaidi. Je, ni kizuri kwa afya yako? Pengine unatumia asali kwa ajili ya kuongezea utamu, au hata unaweza ukawa unatumia asali ya Manuka kwa manufaa yake ya kimatibabu. Ikiwa umewahi kujaribu kula sega la asali, utajua jinsi ile sehemu iliyo laini ilivyo tamu inapoyeyuka kwenye ulimi wako.

Katika Zaburi 119:103,104, mtunga-zaburi anaeleza Biblia kama sega la asali—mfano au sitiari kwa ajili ya kitu kinachopendeza: “Mausia yako ni matamu sana kwangu, kupita asali kinywani mwangu. Kwa mausia yako najipatia ufahamu."

Ndiyo, maneno ya Mungu kwa hakika ni matamu kwa nafsi zetu na tofauti na kitu kingine chochote ambacho ulimwengu unaweza kutupatia. Tofauti na vitindamlo vingi, utamu wa Neno la Mungu ni uponyaji kwa roho zetu na hubadilisha maisha kulingana na tabia zetu. Ikiwa umekuwa mbali na Mungu, unaweza kupiga magoti, kufungua Neno Lake, na kunywa kutoka katika maji yaliyo hai ambayo pekee yatatosheleza.

  • Mungu anawapatia nini wale wanaomjia Yeye ili “wale” kutoka katika Neno Lake?
  • Mwaliko Wake kwako hapa ni upi?
  • Changamoto Yake ni nini?
  • Mwitiko Wake ni Nini?

Neno la Mungu lililo hai na lenye nguvu hukata moja kwa moja kwenye mioyo, akili, na nafsi zetu linapotupatia changamoto ya kukua katika Kristo. Lakini linaweza kufanya hivi kwa ajili yetu tu kwa kiwango ambacho tunachukua muda na jitihada (na ndiyo, hilo linahitaji jitihada) ya kuzama ndani ya Neno kwa mtazamo wa kujisalimisha na unyenyekevu na nia ya kufuata kile linachofundisha.