HomeResourcesSabbath School quarterly

Kuishi Leo

21/06/2026

Tunapotazama pande zote, tunaona ulimwengu ukitetemeka na kuugua, na ishara alizotuambia Yesu zinatimilika mbele ya macho yetu. Vita na uvumi wa vita, mataifa yanayoinuka dhidi ya mataifa mengine, njaa, matetemeko ya ardhi, na mateso (Mt. 24:6—11) yanatokea kote kote na yanaonekana tu kuzidi kadiri wakati unavyosonga. Ndiyo, tunaishi katika nyakati ngumu nyakati tunapohitaji uhusiano wa kudumu pamoja na Mungu.

Tunaambiwa, Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala (1 Pet. 4:7). Ikiwa ni hivyo basi, tena zaidi sana sasa ni wakati wa kuimarisha na kuthibitisha uhusiano wako binafsi na Mungu. Na bila kujali ni muda gani unapita, maisha yetu binafsi siku zote ni mafupi, haidhuru tunaishi kwa muda gani. Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya Biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka (Yakobo 4:13, 14). Tunajua jinsi onyo hilo lilivyo la kweli. Baadhi yenu mnaosoma maneno haya sasa hivi huenda msiwe hai siku hii itakapokuwa ikiisha. Hii ni sehemu ya ukweli wa kusikitisha wa kuishi katika ulimwengu ulioanguka dhambini. Ni muhimu jinsi gani, basi, kuhakikisha uhusiano wetu na Mungu na kuishi daima katika utambuzi wa uhitaji wetu kwake na neema yake inayookoa?

Sisi sote tunahitaji uamsho maishani mwetu. Ni rahisi sana kuridhika au hata kuwa na usahaulifu wa kile ambacho Mungu ametutendea na anatutendea. Ni muumini gani mwaminifu, hata kama anasumbuka na udhaifu fulani, asiyeweza kuomba kama hivi: Uangazishe uso wako nasi tutaokoka! (Zab. 80:19)? Unapokubali kile ambacho Bwana Yesu amekutendea, unapojua kwamba dhambi zako zimesamehewa na kwamba umefunikwa na haki Yake kamilifu, ambayo inahesabiwa kwako kwa njia ya imani, utajua kwamba unaokolewa katika Yeye.