HomeResourcesSabbath School quarterly

Mkao wa Maombi

04/05/2026

Jambo linapoharibika maishani mwetu, wengi wetu huita rafiki wa karibu kulijadili. Tunapokuwa na habari njema, tunatafuta mtu wa kumweleza. Tunaweza kufanya hivyo na Mungu. “Maombi ni kufungua moyo kwa Mungu kama kwa rafiki.” — Ellen G. White, Steps to Christ, uk. 93. Maombi hayadumishi tu uhusiano wetu na Mungu lakini humjulisha mwovu kuwa sisi ni mali ya nani. Tunapopiga magoti kuomba wakati wa asubuhi, ni kama tangazo halisi kwa nguvu za giza kwamba leo tumemchagua Mungu. Si hivyo tu, bali Mungu hutuma malaika kuwa upande wetu tunapoomba, nasi tumezingirwa na kulindwa dhidi ya adui wa giza (Zaburi 91).

Kitendo halisi cha kupiga magoti katika kujisalimisha huonesha mkao wa unyenyekevu. Kwa namna fulani ni tofauti na kukaa kwenye kiti au kulala kitandani wakati tukiomba, ingawa tunaweza pia kuomba tukiwa katika mikao ya jinsi hiyo pia. Hata hivyo, tunapopiga magoti mbele za Mungu, tunaonesha kwamba tuko tayari kumtumikia Mungu kwa mioyo yetu yote, na maneno yetu yanatangaza kwamba yeye ni Mwenye Enzi na kwamba sisi tu watoto wake tuliombwa naye tu.

Kuomba katika hali ya kusimama ilikuwa desturi ya kawaida katika nyakati za Biblia (2 Nya. 20:5, 6, 13; 1 Sam. 1:26; Ayubu 30:20; Lk. 18:11, 13). Biblia pia hutupatia mifano ya watu walioomba hali wameketi (2 Sam. 7:18). Wengine walisujudu mbele za Mungu, nyuso zao zikiwa sakafuni -ingawa mkao huo ulihusishwa na maombi mara chache, basi zaidi sana kujishusha mbele ya mkubwa (1 Fal. 1:47, Mk. 14:35).

Mkao wako wa kawaida wakati wa maombi ni upi? Biblia haitutaki kuomba katika mkao fulani mahususi, lakini mkao ni muhimu, kwa vile unaonesha kicho chetu, hisia zetu za ndani, na shauku yetu ya kujisalimisha kwa Mungu. Baadhi ya watu hawawezi kupiga magoti; kwa hiyo, kilicho muhimu zaidi ni hali ya moyo. Kama unaweza kupiga magoti lakini kwa kawaida hufanyi hivyo, kwa nini usijaribu kupiga magoti wakati mwingine ukiomba na uone inaleta matokeo gani katika muda wako na Mungu.