HomeResourcesSabbath School quarterly
Maswali Mengine Kuhusiana na Maombi
14/05/2026
Kwa nini uombe wakati tayari Mungu anajua? Kwa nini tuombe wakati ambapo Mungu Yuajaa yote? Ellen G. White anafafanua hivi: “Si lazima kufanya hivyo ili kumjulisha Mungu hali yetu ilivyo, bali kuongea naye kunatuwezesha kumpokea mioyoni mwetu. Sala hazimlazimishi Mungu kushuka kwetu, bali ni sisi ambao tunainuliwa mpaka kufika kwake.” _—Jipatie Amani Moyoni, uk. 70. Kwa hakika Mungu anajua shauku zetu na mahitaji yetu, na anasoma kila kusudi la mioyo yetu. Lakini kuomba ni kitu chema kwetu. Maombi yanatualika kukoma katikati ya pilikapilika katika maisha yetu, kutulia na kutambua kwamba Mungu ndiye mtawala wa vyote na kujiweka miguuni Pake. Njia pia zaweza kufunguliwa kwa ajili ya Mungu kutenda ikiwa tutamwalika kufanya hivyo. Roho Mtakatifu hutuombea wakati ambapo hatujui namna ya kuomba tupaswavyo (Rum. 8:26, 27).
Kwa nini uombe wakati yote ni salama? Kujitosheleza na kiburi (taz. Somo la 3) vinaweza kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa kabisa kwa maisha ya maombi thabiti. Ikiwa tu tungetambua ni kiasi gani tunamhitaji Mungu, tungemjia mara nyingi zaidi! Ikiwa malaika wakamilifu wanamsifu na kumwabudu, kwa nini sisi, tulio wanadamu wenye dhambi, tudhani kwamba si wahitaji sana wa maombi? Je, Mathayo 5:6 na Isaya 44:3 zinasema nini juu ya ukweli huu?
Imani ina sehemu gani katika maombi? Soma Waebrania 11:6 kisha utafakari maneno haya: "Maombi na imani vimeshikamana kwa karibu sana, navyo vinapaswa kujifunzwa pamoja. Katika ombi la imani kuna sayansi ya kimbingu ni sayansi ambayo kila anayetaka kufaulu maishani lazima aielewe. Kristo anasema, “Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu" Marko 11:24. Anaweka wazi kuwa kuomba kwetu lazima kuambatane na mapenzi ya Mungu; ni lazima tuombe mambo yale aliyoahidi na tukipokea tutumie kufanya mapenzi Yake. Masharti hayo yakitimizwa, ahadi haina mashaka... Hatuna haja ya kutafuta uthibitisho wa nje wa baraka Zake. —Ellen G. White, Elimu ya Kweli, uk. 210.`
Niombe na Nani? Muda mwingi zaidi tunapaswa kuomba wenyewe (Mungu na wewe tu), kwa vile maombi na kujifunza Biblia ni kama damu ya uhusiano wako na Mungu. Tenga muda wa kuuchunguza moyo wako wakati ukizungumza na kumsikiliza Mungu (Mt. 6:6). Tunapaswa pia kuomba na familia zetu au katika vikundi vidogo (Mdo. 12:12), maana wakusanyikapo wawili au watatu kwa jina Bwana Mungu yupo hapo (Mt. 18:20). Mwisho, tunapaswa kuomba na jumuia zetu za kanisa (Yak. 5:13-16). Maombi ya aina zote tatu ni ya muhimu.
Nisikilizeje? Maombi ni zaidi tu ya kuzungumza na Mungu; tunapaswa pia kumruhusu "atupogoe" na kuzungumza juu ya maisha yetu. Njia bayana kabisa na salama ya kulifanya hili ni kwa kusoma Biblia na kuunganisha maombi na usomaji wa Biblia katika wakati wako wa ibada. Uwe mwangalifu usije ukawa unasikiliza mawazo yako tu badala ya kuchunguza Biblia.