HomeResourcesSabbath School quarterly
Musa, Mtumishi Mnyenyekevu
14/04/2026
Kumbi kubwa za ikulu ya Misri zilidhihirisha utajiri, starehe na anasa. “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo” (Mdo. 7:32) Maisha ya mamlaka, utajiri na umaarufu yalikuwa kwa ajili yake kuyatumia; licha ya hivyo, Musa alichagua kitu kilichokuwa tofauti kabisa. “Kama mwanahistoria, mshairi, mwanafalsafa, jemadari wa majeshi, na mtungasheria anajitokeza pasipo kifani. Na bado pamoja na ulimwengu kuwa mbele yake, alikuwa na nguvu ya kimaadili ya kukataa matarajio ya utajiri na ukuu na umaarufu vyenye ushawishi, “ ‘akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo.’ ” — Ellen G. White, Wazee na Manabii, Sehemu ya Kwanza, uk. 254.
Unyenyekevu wa Musa wa baadaye unastaajabisha, tukimfikiria Yule mtu alivyokuwa mwenye nguvu na alipotokea. Hata hivyo, kupitia tendo lenye msukumo wa dhambi (Kut. 2:12), alipoteza kujiamini na kujitegemea. Akizungukwa na milima kama kuta za darasa lake na kiburi kikiwa kimetupwa pembeni, kwa miaka 40, Musa alifundishwa na Mungu kile alichohitaji kujua ili kuongoza taifa kutoka utumwani na kuingia katika Nchi ya Ahadi. Mamlaka na utajiri wa maisha ambayo yangekuwa tofauti katika Misri vilififia wakati Musa alipozingatia umilele. Mungu alikuwa amemwita kwa uwazi kabisa, na Musa akafuata.
Pengine muhimu zaidi kulingana na mada hii, Hesabu 12:3 inatuambia: “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.” Musa, mmoja wa wazee wa imani wakubwa katika Biblia, anajulikana kwa unyenyekevu wake, upole wake. Fikiria jinsi ambavyo maisha na uongozi wake ungekuwa tofauti kama kiburi kingeingia katika kila moja ya matukio haya makubwa katika maisha yake: kichaka kinachowaka moto, mapigo katika Misri, kuvuka Bahari ya Shamu, kuanguka kwa mana kutoka mbinguni, kuzungumza moja kwa moja kwa Mungu, kupokea Amri Kumi, na kusikia maneno ya Mungu baada ya kuugonga mwamba.