HomeResourcesSabbath School quarterly
Kosa Kubwa Kuliko Yote
15/04/2026
Fikiria kama ungekuwa mwanafunzi wa Bwana Yesu. Ungesafiri Naye, ungekula Naye, ungelala karibu Naye, na kujifunza kutoka Kwake wakati akibadilisha maisha ya watu wengi, yakiwemo maisha yako mwenyewe. Watu wangebanana Naye, na ungetambua jinsi lilivyo jambo la pekee kwamba alikuchagua wewe kuwa mmoja kati ya watu 12 watakaokuwa karibu zaidi na Yeye. Ndipo unatulia ukijiuliza: Ni nani kweli aliye mkuu kati ya wanafunzi wote?
Mtu angeweza kuwaza kwamba baada ya muda wote huu wa kuwa karibu na Yesu, mjadala wa namna hii ungekuwa jambo la mwisho kutarajiwa kuwemo mawazoni mwao. Lakini hilo si lililotokea.
Badala ya watu hawa kuridhishwa na wito wao, kiburi kiliibuka mioyoni mwao kiasi ambacho kila mmoja alijidhania kuwa bora kuliko wengine. Ni rahisi kuruhusu mawazo ya namna hiyo kutawala akili zetu. Lakini tunaambiwa kuwa, “hakuna chukizo kwa Mungu au kitu kilicho cha hatari kwa roho za wanadamu kama kiburi, na kujiona kuwa umetosheka. Katika dhambi zote hi ndiyo isiyo na matumaini, na isiyo na matibabu.” —Lulu za Uzima, uk.101.
Hili ni jambo baya sana kwetu. Kiburi chetu kinamuudhi Mungu zaidi ya kitu kingine chochote, na ni sifa ya tabia ambayo ni vigumu kuishinda kwa sababu mara nyingi hatuioni jinsi ilivyo. Katika hali yetu ya kujitosheleza, tunachagua kutojitathmini, kwani hakika kiburi ni mfalme. Tunahitaji kutulia, tujichunguze, na tumwombe Mungu atufungue macho tuone hali yetu ya kweli, kwani kiburi kinaweza kuwa sababu kuu inayotuzuia kuwa na uhusiano wa karibu na Mungu leo.